ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YAWAHIMIZA WANAFUNZI KUTAMBUA HAKI YA ELIMU NA KUTIMIZA WAJIBU WAO

14 Aug, 2026
THBUB YAWAHIMIZA WANAFUNZI KUTAMBUA HAKI YA ELIMU NA KUTIMIZA WAJIBU WAO

 

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka wanafunzi nchini kutambua kuwa elimu ni haki ya msingi ya kila mtoto, huku ikisisitiza kuwa haki hiyo inapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji, nidhamu na maadili mema. 

Wito huo umetolewa kwa wanafunzi waliotembelea banda la THBUB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro.

Akizungumza na wanafunzi hao, Afisa Uchunguzi Mkuu wa THBUB, Bi. Juliana Laurent, amesema kila mtoto ana haki ya kupata elimu bila ubaguzi, akieleza kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

“Elimu ni haki ya kila mtoto. Serikali, wazazi na jamii wana wajibu wa kuhakikisha mtoto anapata fursa ya kusoma. Hata hivyo, watoto wenyewe wanapaswa kuitumia haki hiyo kwa kujifunza kwa bidii, kuheshimu walimu, kufuata kanuni za shule na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri masomo yao,” amesema Bi. Laurent.

Amefafanua kuwa mtoto pia ana haki ya kusoma katika mazingira salama yanayolinda utu wake, yasiyo na vitendo vya ukatili, unyanyasaji wala ubaguzi. Aidha, amewahimiza wanafunzi kutoa taarifa kwa walimu, wazazi au mamlaka husika wanapokutana na vitendo vinavyokiuka haki zao au za wenzao ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Bi. Laurent ameongeza kuwa utambuzi wa haki za mtoto unapaswa kuambatana na utekelezaji wa wajibu wake, akibainisha kuwa wanafunzi wanapaswa kuheshimu haki za wengine, kushirikiana na wenzao, kutunza mali za shule na kuwa mfano wa maadili mema ndani na nje ya mazingira ya shule.

Kwa upande wao, wanafunzi waliotembelea banda la THBUB wamesema elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu haki zao na kuwapa hamasa ya kutekeleza wajibu wao kwa bidii. Wameeleza kuwa wataendelea kuwa mabalozi wa haki za watoto katika shule zao na katika jamii wanamoishi.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane, THBUB inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga jamii inayotambua, kuheshimu na kulinda haki za binadamu, sambamba na kuhimiza uwajibikaji wa kila mwananchi katika maendeleo ya taifa

slot gacor