TUME KUCHUNGUZA MALALAMIKO YA WANANCHI KATA YA KATUBUKA

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Amina Talib Ali amesema THBUB imepokea malalamiko ya Wananchi wa Kata ya Katubuka kuhusiana na masuala mbalimbali ya uvunjifu wa haki za Binadamu na ukiukwaji wa misingi ya Utawala bora.
Mhe. Amina amesema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Katubuka katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Katubuka Manispaa ya Kigoma Februari 11, 2025.
Akizungumza baada ya mkutano huo Mhe. Amina amesema miongoni mwa majukumu ya THBUB ni kupokea malalamiko ya Wananchi na kuyafanyia uchunguzi wa kina na baadaye kupeleka mapendekezo kwenye Mamlaka husika ili majibu yapatikane ndani ya siku 90.
"Haki ya mtu huchelewa tu, haki ya mtu haiwezi kupokonywa, tuko hapa kwa ajili ya kuwasikiliza na kuchukua maoni, kero na malalamiko yenu ili kila mmoja apate haki yake" amesisitiza Mhe. Amina.
Katika mkutano huo Wananchi wa Kata hiyo walipata nafasi ya kueleza kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo changamoto ya miundombinu ya Barabara ya kwenda uwanja wa Ndege wa Kigoma na mafuriko ya Maji katika baadhi ya maeneo huku wakiomba Serikali kufanyia kazi kero hizo ili kuwaondolea bughudha.