UELEWA WA HAKI ZA BINADAMU WATAJWA KUWA MSINGI WA KUJENGA JAMII INAYOWAJIBIKA.
Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Happy Mtei, amewahimiza wanafunzi kujifunza na kuzielewa haki za binadamu sambamba na kutimiza wajibu wao kwa kuwa hatua hiyo itawajengea uwezo wa kujilinda, kuwasaidia wazazi wao na kuwa walinzi wa haki katika jamii.
Bi. Mtei ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati wa ufunguzi wa Klabu za Haki za Binadamu katika Shule ya Sekondari Diplomasia na Shule ya Msingi Kiungani.
Akizungumza na wanafunzi hao , Bi. Mtei amesema elimu ya haki za binadamu huwajengea uwezo wa kuzitambua, kulinda na kutetea haki zao na za wengine na amesisitiza kuwa elimu ya haki hizo ndiyo msingi wa kujenga jamii inayoheshimu utu, usawa na uwajibikaji.
Aidha, Bi. Mtei amesema kuwa kuanzishwa kwa Klabu za Haki za Binadamu kutawapa wanafunzi fursa ya kujifunza haki na wajibu wao, kutambua viashiria vya ukiukwaji wa haki za binadamu na kuwa mabalozi wa kuhamasisha utamaduni wa kuheshimu haki hizo shuleni na katika jamii.
Naye Mwalimu Abdullah Mshana akizungumzia umuhimu klabu ya haki za binadamu, amesema kuwa kuanzishwa kwa klabu hiyo kutasaidia kupunguza tatizo la utoro miongoni mwa wanafunzi kwa kuwajengea uelewa wa umuhimu wa elimu, nidhamu na kutekeleza wajibu wao wa kuhudhuria masomo.
Klabu ya haki za binadamu katika shule za msingi, secondari na vyuo ni jukwaa muhimu katika kuwajengea watoto na vijana utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

