WANAFUNZI WAASWA KUWA WAZALENDO
Wanafunzi nchini wametakiwa kujenga moyo wa uzalendo, kuipenda nchi yao na kutimiza wajibu wao kama msingi wa kulinda haki za binadamu na kuimarisha misingi ya utawala bora.
Wito huo umetolewa na Afisa Uchunguzi Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Bi. Florence Chaki, wakati akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dar es Salaam waliotembelea banda la Tume katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam Julai 9, 2025.
Akitoa elimu kwa wanafunzi hao, amesema kuwa haki na wajibu haviwezi kutenganishwa, hivyo ni muhimu kwa watoto na vijana kutambua wajibu wao kwa familia, shule na taifa ili waweze kuelewa, kulinda na kudai haki zao kwa njia sahihi.
Bi. Florance aliwakumbusha kuwa uzalendo, uadilifu, kuheshimu sheria na kuwajibika ni nguzo muhimu zinazochangia ulinzi wa haki za binadamu na ujenzi wa jamii inayoheshimu haki za binadamu na misingi imara ya utawala bora.
“Mtoto anayefahamu wajibu wake hukua akiwa raia mwema, anayeheshimu sheria na kuchangia maendeleo katika nchi yake” alisema Bi. Chaki.
Kwa niaba ya wanafunzi waliotembelea banda la THBUB, mwanafunzi Samira Ismail, alisema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa kuwa uzalendo na kutimiza wajibu ni nguzo muhimu katika kulinda haki za binadamu. Alisema wao kama wanafunzi wataendelea kuwa mabalozi wa elimu hiyo kwa wenzao shuleni na katika jamii ili kujenga kizazi kinachozingatia haki, wajibu na maadili mema.

