MEYA WA JIJI LA DODOMA AIPONGEZA THBUB KWA KUTOA ELIMU YA HAKI ZA BINADAMU.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Mhe. Alimwoni Chaula ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa juhudi zake za kuelimisha wananchi kuhusu haki za binadamu kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maeneo tofauti nchini.
Mhe. Chaula alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la THBUB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo kwa wananchi.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Chaula alisema ameridhishwa na kazi inayofanywa na THBUB ya kufikisha elimu ya haki za binadamu kwa wananchi katika mikoa mbalimbali nchini.
“Mnafanya kazi nzuri, kazi zenu naziona mnajitahidi sana , kwenda mikoa mbalimbali. Hongereni sana, mnafanya kazi nzuri ya kutoa elimu kwani hakuna kitu kikubwa kama haki za binadamu “ alisema Mhe. Chaula.
Aidha, Mhe. Chaula amesisitiza kuwa elimu ya haki za binadamu ina mchango mkubwa katika kujenga jamii inayotambua wajibu na haki zake, hivyo kuimarisha utawala bora, amani na maendeleo ya taifa.
Kwa upande wa THBUB , Afisa Uchunguzi Mkuu Bw. Aristarico Majura akielezea umuhimu wa wadau katika kulinda haki za binadamu nchin, amesema THBUN itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na elimu ya haki za binadamu, sambamba na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kulinda na kutetea haki hizo.
Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuwasilisha huduma, bidhaa na mipango yao kwa wananchi, huku yakitoa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuongeza uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.

