MKUU WA MKOA AWATAKA WAAJIRI KUZINGATIA MASLAHI YA WAFANYAKAZI
Wafanyakazi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wameungana na wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani, wakiahidi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, uwajibikaji na kwa kuzingatia misingi ya haki na utawala bora.
Maadhimisho hayo yamefanyika Mei 1, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, yakihudhuriwa na mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Chalamila aliwataka waajiri nchini kuzingatia maslahi ya wafanyakazi kwa kuwapatia haki zao stahiki pamoja na kuhakikisha wanakuwa na mazingira bora ya kazi. Alisisitiza kuwa hatua hiyo itaongeza ustawi wa wafanyakazi na kuimarisha ufanisi katika taasisi.
Aidha, aliwakumbusha waajiri wajibu wao wa kuzingatia sheria za kazi na kutoa stahiki muhimu kwa wafanyakazi, huku akibainisha kuwa wafanyakazi wanapothaminiwa huchangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya taasisi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao, wafanyakazi wa THBUB wamesema maadhimisho hayo yamewapa nafasi ya kutafakari mchango wao katika kulinda na kuendeleza haki za binadamu pamoja na kuimarisha utawala bora nchini. Wameahidi kuongeza juhudi katika utendaji kazi wao ili kufikia malengo ya taasisi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Sambamba na hilo, wafanyakazi hao wamehimizwa kuzingatia maadili ya kazi, nidhamu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, wakielezwa kuwa bidii na uadilifu ni msingi wa kuongeza tija na kukuza uchumi.
Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo: “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”
Kupitia maadhimisho hayo, THBUB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kusimamia haki za binadamu, uwazi na uwajibikaji, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kujenga jamii yenye usawa na maendeleo endelevu.

