MPANGO KAZI WA KITAIFA WA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA KUCHOCHEA MAENDELEO

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi na Uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara, Mzee Ali Haji, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, amesema kuwa rasimu ya mpango kazi huo inalenga kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa ipasavyo katika maeneo yote ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikako cha tano (5) cha Kamati hiyo kilichofanyika katika hoteli ya Four Points, Jijini Dar es salaam, Juni 4, 2025, Mzee Haji alisema kuwa mpango kazi huu unalenga kuimarisha sekta za utalii, uchumi wa buluu, viwanda, biashara, madini na uwekezaji kwa kuzingatia haki za binadamu.
Aidha, Mzee Haji alieleza kuwa rasimu hiyo imechambua kwa kina masuala ya haki katika sekta za viwanda, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Kazi, mazingira salama ya kazi na kukomesha unyanyasaji kazini.
Mzee Haji alimaliza kwa kusema kuwa rasimu hiyo imekamilika mara baada ya kazi nzuri iliyofanywa na timu ya wataalamu ya kuunganisha mapendekezo yote yaliyojadiliwa na Kamati Kuu ya Kitaifa pamoja na kupokea maoni ya wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali na taasisi binafsi.
Rasimu ya mpango kazi huo inatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kuanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo matarajio ya Serikali ni kwamba, kupitia utekelezaji wake, kila mwananchi atakuwa na uhakika wa kufanya kazi katika mazingira ya haki, usawa na ulinzi wa Sheria za kitaifa na kimataifa.