ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YAENDELEA KUTATUA KERO ZA WANYONGE BURE.

14 May, 2026
THBUB YAENDELEA KUTATUA KERO ZA WANYONGE BURE.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imebaini kuwa idadi kubwa ya Wananchi Mkoani Dodoma bado wanakabiliwa na uelewa mdogo wa haki zao za msingi, jambo linalochangia kuchelewa kupata haki au kufanyiwa uonevu katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu Mei 11, 2026, ikiwa ni siku ya 11 tangu kuanza kwa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Mchunguzi Mkuu Msaidizi wa THBUB, Bw. Halfan Botea, amesema Tume imejipanga vizuri kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi.

Bw. Botea ameeleza kuwa tangu kuanza kwa kampeni hiyo mkoani Dodoma, Tume imekuwa ikipokea wananchi wengi wenye kero tofauti, ambapo hadi sasa jumla ya malalamiko 33 yameshawasilishwa katika mabanda ya Tume hiyo yaliyopo Dodoma na Shinyanga.

"Kufikia sasa tayari tumekusanya malalamiko 33, ambapo matano kati ya hayo yameshapatiwa ufumbuzi wa papo kwa hapo na mengine yaliyosalia yanaendelea kushughulikiwa na Tume kwa mujibu wa sheria na taratibu zetu," alisema Bw. Botea.

Takwimu za Tume hiyo zinaonyesha kuwa changamoto kuu zinazowasumbua wananchi wa Dodoma ni pamoja na: Migogoro ya ardhi, uvamizi na dhuluma za maeneo ya ardhi, mirathi na ndoa, ugomvi wa mali za marehemu, matunzo ya watoto, ukiukwaji wa haki za wafanyakazi mahali pa kazi, ukatili wa kijinsia, na mashauri yanayohusu ukatili ndani ya jamii.

Bw. Botea amesema mbali na kupokea malalamiko, Tume imeweza kutoa elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa wananchi 69 waliofika bandani hapo.

Aidha, Bw. Botea amebainisha kuwa wamebaini elimu ndogo kwa wananchi kuhusu haki za binadamu na utawala; wengi hawafahamu haki zao za msingi na hawajui mamlaka sahihi ya kushughulikia kero zao. Kupitia kampeni hii THBUB inatoa dira ili mwananchi ajue pa kwenda kuanzia ngazi ya kata hadi kitaifa.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inatoa fursa adhimu kwa wananchi kupata msaada wa kisheria bila malipo yoyote, lengo likiwa ni kurejesha misingi ya haki na utawala bora kwa kila Mtanzania.

slot gacor