THBUB YAENDELEA KUTOA ELIMU YA HAKI ZA BINADAMU KUPITIA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA SHINYANGA.
Wakazi wa Shinyanga na maeneo ya jirani wameendelea kunufaika na huduma ya kuwasilisha malalamiko ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora pamoja na elimu ya haki za binadamu.
Huduma hii imetolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora katika banda la ofisi hiyo wakati wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayofanyika katika Viwanja vya Nguzo Nane Mkoani Shinyanga.
Kupitia kampeni hiyo, wakazi hao wamepata fursa ya kuwasilisha malalamiko yao na kuelimishwa kuhusu haki zao za msingi ili kujengewa uwezo wa kufahamu haki zao ikiwa ni juhudi za kujenga jamii inayozingatia haki, usawa, amani na maendeleo.
Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo, Afisa Mfawidhi wa tawi la THBUB Mwanza anayehudumia mikoa iliyopo Kanda ya Ziwa, Bw. Gordian Binamungu amesema kuwa Tume inasisitiza wananchi kuendelea kupata elimu ya haki za binadamu na utawala bora ili waweze kuzifahamu na kuzidai haki zao kwa mujibu wa sheria.
“Kupitia kauli mbiu ya msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo, sisi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora tunatoa huduma bure na tunasisitiza wananchi waendelee kupata elimu ya haki za binadamu ili wazifahamu haki zao za msingi,” amesema Binamungu.
Sambamba na huduma zinazotolewa katika banda la THBUB , elimu hiyo imetolewa pia kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Masekelo kuhusu haki za binadamu, utawala bora na umuhimu wa kuanzishwa kwa Klabu za Haki za Binadamu mashuleni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tume katika kuwajengea vijana uelewa wa haki, wajibu na maadili ya utawala bora tangu wakiwa shuleni.

