ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YAITAKA SERIKALI NA WAAJIRI NCHINI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA BORA YA KAZI

14 May, 2025
THBUB YAITAKA SERIKALI NA WAAJIRI NCHINI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA BORA YA KAZI

 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeitaka serikali na waajiri wote nchini kuendelea kuweka mazingira bora ya kazi na kusimamia maslahi ya wafanyakazi kwa mjibu wa katiba na sheria za Ajira ili kujenga mazingira rafiki kwa wafanyakazi kufurahia haki zao za kufanya kazi.

Rai hiyo imetolewa na Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji Mstaafu), Mwenyekiti wa THBUB alipokuwa akizungumza na Vyombo vya habari katika kuelekea maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani Aprili 30, 2025 Jijini Dodoma.

Mhe. Mwaimu amesema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kutambua mchango wa wafanyakazi duniani kote katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Nitoe rai kwa serikali na waajiri wote nchini kuendelea kuweka mazingira bora ya kazi na kusimamia vyema maslahi ya wafanya kazi kwa mjibu wa Katiba na Sheria za Ajira ilikujenga mazingira rafiki kwa wafanyakazi kufurahia haki yao ya kufanya kazi na pia kuleta tija na ufanisi katika utendaji, ”amesema.

“Maadhimisho haya  ya Mei Mosi mwaka 2025 yalienda sambamba na kaulimbiu isemayo “Uchaguzi mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali Haki na maslahi ya wafanyakazi,sote tushiriki uchaguzi”

Mhe. Mwaimu amesisitiza kuwa kaulimbiu hiyo inawahamasisha wafanyakazi kujitokeza kushiriki uchaguzi huo ili kuhakikisha kwamba pamoja na wananchi wengine wanashiriki kikamilifu kuwachagua viongozi wenye kusimamia na kulinda haki za binadamu.

Aidha, Mhe. Mwaimu amesema THBUB inatambua na kupongeza juhudi za serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kuhakikisha nchi inapata viongozi waadilifu, wasiyo na ubaguzi, wenye uzalendo, wanaoheshimu haki za Binadamu na na kuzingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuendelea kujenga Taifa lenye amani na utulivu.