THBUB YASHIRIKI KIKAO CHA TUME YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imeshiriki kikao cha themanini na saba (87) cha Haki za Binadamu Jijini Banjul nchini Gambia kuanzia tarehe 11 hadi 20 Mei, 2026. Kikao hicho kimejikita katika kujadili masuala yahusuyo ulinzi wa haki za binadamu, utawala bora, na utekelezaji wa mikataba ya kikanda barani Afrika.
Akizungumza leo tarehe 19 Mei, 2026 Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka THBUB, Bi. Ellen Rwijage ameeleza kuwa kikao hicho huwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za kitaifa za haki za binadamu, serikali, mashirika ya kiraia na wataalamu wa sheria ambapo hujadili changamoto na mafanikio katika kulinda haki za binadamu na watu.
”Vikao hivi ni muhimu sana, kama nchi tunapata muda wa kujadili masuala yahusuyo haki za binadamu, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya haki na utawala bora ambayo kwetu sisi ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira 2050.” Amesema Bi. Rwijage.
Aidha, Bi. Rwijage ameeleza kuwa malengo ya kikao hicho cha 87 kwa kiasi kikubwa yanaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 huku akitaja baadhi ya maeneo ambayo dira imeweka msisitizo ni pamoja na utawala bora, utawala wa sheria, na ulinzi wa haki za binadamu.
Ushiriki wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika vikao hivyo ni sehemu ya kutekeleza wajibu wa kimataifa na kikanda wa kulinda haki za binadamu na kuimarisha utawala bora.

