THBUB YATOA ELIMU YA HAKI ZA BINADAMU KWA WATUMISHI WA HALMASHAURI YA NZEGA
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Tawi la Tabora, imetoa elimu kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu haki, wajibu na umuhimu wa kuzingatia sheria, uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Elimu hiyo imetolewa na maafisa wa Tume, Raphael Mavunde, Afisa Mchunguzi Mkuu, na Simon Hillonga, Afisa Sheria, ambao wamefafanua majukumu ya THBUB katika kukuza na kulinda haki za binadamu pamoja na kuimarisha utawala bora nchini.
Katika mafunzo hayo, watumishi wameelezwa kuwa haki za binadamu ni za kila mtu bila ubaguzi wa rangi, kabila, jinsia, dini au hali yake katika jamii. Pia, wamepata ufafanuzi kuhusu haki na wajibu wa wananchi kwa kuzingatia Ibara ya 25 hadi 28 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia misingi ya utawala bora, Mavunde na Hillonga wameeleza umuhimu wa ushirikishwaji, uwazi, utawala wa sheria, uadilifu na uwajibikaji katika matumizi ya mamlaka na utekelezaji wa majukumu ya umma.
Aidha, watumishi wamefahamishwa kuhusu majukumu ya Tume, yakiwemo kupokea na kuchunguza malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu, kutoa elimu na ushauri wa kisheria, kufanya tafiti na kutembelea maeneo ya vizuizi, ikiwemo mahabusu, kwa ajili ya kufuatilia hali ya haki za watu wanaoshikiliwa. Pia, wameelekezwa namna ya kuwasilisha malalamiko kwa Tume kupitia barua au kufika moja kwa moja katika ofisi zake.
Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwajibikaji na weledi kwa watumishi wa umma, ili haki za binadamu na misingi ya utawala bora zisiwe dhana ya kinadharia pekee, bali zionekane katika utendaji wa kila siku na utoaji wa huduma zinazozingatia haki, usawa na sheria kwa wananchi

