ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB YAWAJENGEA UWEZO WALEZI WA KLABU ZA HAKI ZA BINADAMU DAR ES SALAAM.

22 May, 2026
THBUB YAWAJENGEA UWEZO WALEZI WA KLABU ZA HAKI ZA BINADAMU DAR ES SALAAM.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Tawi la Dar es Salaam, imeendesha mafunzo kwa walimu walezi wa Klabu za Haki za Binadamu kutoka shule mbalimbali za mkoa huo kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu haki za watoto na namna bora ya kuendesha klabu hizo mashuleni.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Afisa Mfawidhi wa THBUB Tawi la Dar es Salaam, Bi. Shoma Philip, Mei 22, 2026 katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya THBUB Dar es salaam, ambaye amesema walimu wana nafasi muhimu katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya haki, utu, uwajibikaji na kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili pamoja na ukiukwaji wa haki zao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bi. Philip amesema klabu za haki za binadamu ni nyenzo muhimu katika kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu haki zao, wajibu wao na umuhimu wa kuheshimu haki za wengine katika jamii.

“Mtoto anayejua haki zake ana uwezo wa kuzitetea na pia kuheshimu haki za wengine. Hivyo klabu hizi zitasaidia kujenga kizazi chenye maadili mema, amani na uwajibikaji,” amesema Bi. Philip.

Aidha, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha walimu kuelewa kwa kina majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na kuwapatia maarifa kuhusu mwongozo wa uendeshaji wa Klabu za Haki za Binadamu ambazo tayari zimeanzishwa katika baadhi ya shule.

Bi. Philip amewasihi washiriki kutumia nafasi hiyo kujifunza, kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika kuhakikisha klabu hizo zinakuwa imara, endelevu na zenye manufaa kwa wanafunzi pamoja na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya washiriki, Mwalimu Ashura Nyika kutoka Shule ya Msingi Umoja wa Mataifa ameishukuru THBUB kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yatawasaidia walimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika malezi na ulinzi wa haki za watoto mashuleni. Ameahidi kuwa walimu wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa THBUB ili kuhakikisha elimu ya haki za binadamu inaendelea kuwafikia wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, washiriki wa mafunzo hayo walipata fursa ya kutembelea ofisi za THBUB Tawi la Dar es Salaam ambapo walijionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Tume. Washiriki hao walitembelea Dawati la Jinsia na Watoto na kupata maelezo kuhusu namna dawati hilo linavyoshughulikia malalamiko yanayohusu ukatili wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za watoto. Aidha, walitembelea maktaba ya ofisi hiyo na kujifunza kuhusu nyaraka mbalimbali za haki za binadamu na utawala bora zinazotumika kutoa elimu kwa wananchi.

slot gacor