TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAHIMIZA ULINZI WA HAKI ZA RAIA NA WAJIBU WAO KWA TAIFA
Mchunguzi Mkuu Msaidizi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Botea Halfani, amewahakikishia wananchi kuwa taasisi hiyo inaendelea kusimamia na kulinda haki za binadamu kwa mujibu wa sheria za nchi, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutimiza wajibu wao kwa taifa.
Akizungumza katika kipindi cha redio cha AFM 92.9 jijini Dodoma, Botea amesema kuwa Tume ina jukumu la kupokea na kuchunguza malalamiko yote yanayohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu, pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki zao za msingi.
Amesema kuwa haki za binadamu zinajumuisha haki ya kuishi, haki ya kupata elimu, haki ya uhuru wa mawazo, pamoja na haki ya kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji. Aidha, anasisitiza kuwa makundi maalum kama wanawake na watoto yanahitaji ulinzi wa ziada ili kuhakikisha yanapata haki zao kikamilifu.
Katika mazungumzo hayo, amebainisha kuwa sheria mbalimbali zimewekwa ili kulinda haki hizo, ikiwemo sheria zinazohusu makosa ya jinai, makundi maalumu pamoja na ulinzi wa watoto. Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kufahamu sheria hizo ili kujilinda na pia kushiriki katika kutoa taarifa pindi wanapoona ukiukwaji wa haki.
Pamoja na hayo, Botea ametaja wajibu wa raia kwa taifa lao, akisisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba. Aidha, wajibu huo unajumuisha kufanya kazi kwa bidii kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Katiba, kulinda usalama wa taifa, kulipa kodi na tozo mbalimbali, kutii sheria na Katiba ya nchi, kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia pamoja na kulinda na kuhifadhi mazingira.
Botea anasisitiza kuwa ulinzi wa haki za binadamu unaenda sambamba na utekelezaji wa wajibu wa raia, na kwamba jamii haiwezi kuwa na haki bila uwajibikaji wa wananchi wake, na kuwahimiza wananchi kutumia njia halali kuwasilisha malalamiko yao kwa Tume ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatoa wito kwa wananchi wote kutambua kuwa haki na wajibu ni pande mbili zisizotenganishwa katika kujenga taifa imara. Kila mwananchi anapaswa si tu kudai haki zake, bali pia kutimiza wajibu wake kwa uadilifu na uzalendo. Ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na taasisi za serikali utachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utawala bora, kulinda utu wa binadamu na kudumisha amani ya kudumu. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi inayoheshimu haki, sheria na misingi ya haki kwa wote.

