WAFANYAKAZI WA THBUB MWANZA WASHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI MISUNGWI.
Wafanyakazi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) tawi la Mwanza Mei 1, 2026 wameungana na wafanyakazi wengine mkoani Mwanza katika maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Maadhimisho hayo yameongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda ambaye alikuwa mgeni rasmi, huku yakibebwa na kauli mbiu isemayo “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mtanda aliwataka wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuchochea maendeleo ya taifa.
“Wafanyakazi ndiyo nguvu kubwa ya maendeleo ya taifa letu, hivyo ni muhimu kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa weledi na kuwajibika,” alisema Mhe. Mtanda.
Aidha, aliwahimiza waajiri kuendelea kuzingatia sheria za kazi, kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki na stahiki zao kwa wakati.
Katika maadhimisho hayo, wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi walishiriki maandamano, burudani pamoja na shughuli mbalimbali zilizolenga kuonesha mshikamano na kuthamini mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, THBUB Mwanza imesema ushiriki wao katika maadhimisho hayo unaonesha dhamira ya taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutetea haki, ustawi na mazingira bora kwa wafanyakazi na jamii kwa ujumla.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 1 Mei duniani kote kwa lengo la kutambua mchango wa wafanyakazi pamoja na kujadili masuala yanayohusu haki na ustawi wao.

