WANAFUNZI WANUFAIKA NA KLABU ZA HAKI ZA BINADAMU.
Wanafunzi 767 kutoka shule tisa za msingi na sekondari katika mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara wamejiunga na Klabu za Haki za Binadamu zilizoanzishwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) katika kipindi cha Aprili hadi Mei 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu ya haki za binadamu kwa watoto na vijana mashuleni.
Kwa mujibu wa takwimu za utekelezaji wa mpango huo, Mkoa wa Lindi umefanikiwa kupata wanafunzi 123 wa shule za sekondari waliojiunga na klabu hizo, huku Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ikiwa na wanafunzi 447 waliojiunga. Aidha, Mkoa wa Mtwara umeandikisha wanafunzi 240 wa shule za msingi pamoja na wanafunzi 80 wa shule za sekondari waliojiunga katika klabu hizo.
Akizungumzia utekelezaji wa mpango huo, Afisa Mfawidhi wa THBUB Tawi la Mtwara, Juma Mleli, amesema klabu hizo zimekuwa chachu ya kuwajengea wanafunzi uelewa mpana kuhusu haki za binadamu, wajibu wa raia, misingi ya utawala bora pamoja na umuhimu wa kuzingatia maadili mema katika mazingira ya shule na jamii inayowazunguka.
Amesema kupitia klabu hizo wanafunzi wanapata nafasi ya kushiriki mijadala mbalimbali, elimu rika pamoja na shughuli zinazohamasisha amani, usawa, uwajibikaji na utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo, jambo linalosaidia kuwajenga kuwa mabalozi wa haki za binadamu katika jamii.
Bw. Mleli ameongeza kuwa uwekezaji katika elimu ya haki za binadamu kwa vijana ni msingi muhimu wa kujenga jamii yenye uelewa, mshikamano na maendeleo endelevu, huku akizihimiza shule nyingi zaidi nchini kuanzisha Klabu za Haki za Binadamu ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kuendelea kukuza utamaduni wa kuheshimu haki, wajibu na misingi ya utawala bora tangu wakiwa mashuleni.

