WATUMISHI TEKELEZENI MAJUKUMU YENU KWA WELEDI
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bw. Jackson Nyamwihula, amewataka watumishi wa Tume kuwajibika ipasavyo katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa.
Bw. Nyamwihula alieleza hayo wakati wa ziara yake katika Ofisi ya THBUB tawi la Mwanza hivi karibuni.
Alisisitiza kuwa uwajibikaji, uadilifu na nidhamu ni nguzo muhimu katika kuimarisha utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, Bw. Nyamwihula amewakumbusha watumishi kuzingatia maadili ya kazi kwa kuhudumia wateja kwa heshima na weledi, kuheshimu mamlaka, na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Naye, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la THBUB, Bw. Pontian Kitorobombo, alie ambatana katika ziara hiyo,alitoa elimu kwa watumishi kuhusu utaratibu wa kujiunga na chama hicho pamoja na manufaa ya uanachama, ikiwemo kushiriki katika mfuko wa kufarijiana.
“ Pamoja na kufanya kazi kwa ufanisi tunapaswa kuzingatia umuhimu wa kujiunga na TUGHE chama kinachoweza kukutetea na kukulea Mtumishi pale inapobidi” Alisema Bw. Kitorobombo.
Ziara hiyo imeimarisha msisitizo wa uwajibikaji, maadili na mshikamano miongoni mwa watumishi, hatua itakayochangia kuongeza ufanisi na kuendeleza huduma bora kwa jamii.

