ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

WATUMISHI THBUB WATAKIWA KUTOA HUDUMA BORA

27 Apr, 2023
WATUMISHI THBUB WATAKIWA KUTOA HUDUMA BORA

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bwana Patience Ntwina amewataka watumishi wa Tume kuijua vyema taasisi yao na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Pia, ametoa wito kwa waajiriwa wapya kuwa na ushirikiano kazini, kutunza siri za ofisi, kuwa wavumilivu, na kuushirikisha uongozi pindi wapatapo changamoto.

Akifungua mafunzo ya siku nne ya waajiriwa wapya Aprili 24, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi huko Njedengwa Jijini Dodoma, Bwana Ntwina alisema kuwa kila mtumishi wa Tume anao wajibu wa kuifahamu taasisi na majukumu yake ili kuwa na uwelewa wa kutosha na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaowahudumia.

“Baadhi ya watumishi wanayafahamu majukumu ya idara zao tu, lakini ufahamu wao ni mdogo juu ya majukumu ya taasisi, hili halikubaliki,” Bwana Ntwina alisema, na kuongeza kuwa “ni wajibu wa kila mtumishi hapa Tume kujua majukumu ya taasisi yetu.”

Katibu Mtendaji aliwaeleza washiriki kuwa mafunzo hayo ni kama kioo kinachowasaidia kutazama utendaji wao wa kazi iwapo wanafuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma au la; Hivyo, aliwasihi kusikiliza kwa makini mada zote zitakazowasilishwa.

“Ni matumaini yangu kuwa mtazingatia mada zote zitakazotolewa katika mafunzo haya ili kuleta tija katika utendaji wenu wa kazi kwa maslahi ya Tume na Taifa kwa ujumla,” Bwana Ntwina alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Utawala, Bibi Portacia Benito alimshukuru Katibu Mtendaji kwa nasaha zake nzuri kwa waajiriwa wapya na watumishi wote wa Tume na kwa kufungua mafunzo hayo.

Jumla ya Waajiriwa wapya tisa kutoka makao makuu ya Tume Dodoma watanufaika na mafunzo hayo, ambapo mada mbalimbali, zikiwemo: Muundo wa Serikali na uendeshaji wake, Kanuni za utumishi wa umma, huduma bora kwa mteja na nyinginezo zitatolewa.