WATUMISHI WAPYA THBUB WAPATIWA MAFUNZO ELEKEZI YA UTUMISHI WA UMMA.
Watumishi wapya 21 wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kutoka Makao Makuu Dodoma wamepatiwa mafunzo elekezi ya awali kwa muda wa siku nne yaliyotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), kuanzia Mei 19 hadi 22, 2026 Jijini Dodoma. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo kuhusu maadili ya utumishi wa umma, nidhamu kazini, utoaji wa huduma bora, masuala ya afya pamoja na uwekezaji ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Mafunzo ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi na Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala wa TPSC Singida, Martin Lunogelo Fute, amewataka watumishi hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia maadili ya utumishi wa umma ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwajibikaji.
Bw. Fute amesema mtumishi bora wa umma anapaswa kufuata sheria na taratibu za kazi ili kutoa huduma sahihi kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kuitambua taasisi yake, kuielewa mifumo yake ya kazi na kuhakikisha huduma zinazotolewa zina matokeo chanya kwa jamii.
Akifunga rasmi mafunzo hayo Ijumaa Mei 22, 2026, Katibu Mtendaji wa THBUB, Patience Ntwina, amewashukuru wawezeshaji kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa kutoa mafunzo yenye tija kwa watumishi hao wapya, huku akiwataka washiriki kuyazingatia na kuyafanyia kazi yote waliyojifunza ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Hongereni sana kwa kushiriki mafunzo haya kwa uaminifu. Ni muhimu kutenda haki, kuzingatia sheria na kuleta matokeo chanya kwa taasisi katika kuwahudumia wananchi,” amesema Bw. Ntwina.
Kwa upande wao, baadhi ya watumishi waliopatiwa mafunzo hayo wameushukuru uongozi wa THBUB pamoja na wawezeshaji kutoka TPSC kwa elimu waliyoipata kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, David Piniel, amesema utumishi wa umma ni dhamana ya kuwahudumia wananchi na si fursa ya kujinufaisha binafsi, akirejea kauli ya Hayati Julius Kambarage Nyerere kuwa uongozi wa kweli unapaswa kujengwa katika misingi ya kujitolea, uadilifu na usawa kwa wananchi wote.

