Mhe. Dunford George Mpelumbe
Wasifu
Mhe. Wakili Dunford George Mpelumbe ni mwanasheria, mtaalamu wa masuala ya haki za binadamu na sera za umma, mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya sheria, Bunge, utawala wa umma, mahusiano ya kimataifa na utawala bora. Aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 28 Oktoba 2026.
Mhe. Wakili Mpelumbe amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za ndani ya Serikali, Bunge na taasisi za kimataifa. Uzoefu wake wa kazi unajumuisha kuhudumu akiwa Msaidizi Maalumu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anayeshughulikia Masuala ya Sheria za Kimataifa, Mwanasheria wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mshauri wa Sheria katika Wizara ya Nishati, Katibu wa Waziri wa Nishati, pamoja na Msaidizi wa Katibu wa Bunge na Katibu wa Kamati za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihudumu katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Aidha, amewahi kufanya kazi na Jumuiya ya Mabunge ya Madola katika katika Makao Makuu ya Kanda ya Afrika na Makao Makuu Jijini London. Pia amewahi kuwa Mshauri wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akijikita katika masuala ya ulinzi wa mashahidi na waathirika wa uhalifu. Katika hatua za awali za taaluma yake, alihudumu akiwa Mhadhiri Msaidizi wa Sheria za Kimataifa za Umma na Haki za Binadamu katika Chuo Kikuu cha Iringa.
Aidha, Mhe. Wakili Mpelumbe ana Shahada ya Sheria (LL. B) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Masomo ya Siasa za Kimataifa na Mahusiano ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Malmo, nchini Sweden pamoja na Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Sera na Utendaji wa Haki za Binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Roehampton, nchini Uingereza. Pia ana Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M) katika Sheria za Mafuta na Gesi kutoka Chuo Kikuu cha Aberdeen, nchini Scotland na Stashahada ya Mafunzo ya Uanasheria kutoka Shule ya Sheria Tanzania. Aidha, amepata mafunzo mbalimbali ya kitaaluma katika maeneo ya haki za binadamu, usuluhishi wa migogoro ya kimataifa, usimamizi wa rasilimali za mafuta, gesi na madini, sheria na sera za biashara, pamoja na ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Wakili Mpelumbe ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na mwanachama wa Jukwaa la Waamuzi Chipukizi wa Usuluhishi wa Migogoro Afrika). Pia ni mjumbe wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji na ameshiriki katika kamati na vikosi kazi mbalimbali vya Serikali vilivyoshughulikia masuala ya marekebisho ya sheria, mifumo ya udhibiti na usimamizi wa rasilimali za taifa.
Ana utaalamu na uzoefu mkubwa katika nyanja mbalimbali zinazohusisha ulinzi wa haki za binadamu, Katiba na Utawala wa sheria, maboresho ya sheria, upatikanaji wa taarifa, msaada wa kisheria, ulinzi wa wakimbizi, haki za kimataifa za jinai, uwajibikaji wa taasisi na utawala wa kidemokrasia. Kwa kuwa Mwenyekiti wa THBUB, uzoefu wake mkubwa wa kisheria na kiutendaji unasaidia Tume katika kuendeleza jukumu lake la kukuza na kulinda haki za binadamu pamoja na kuimarisha misingi ya utawala bora nchini Tanzania.

