THBUB YATOA WITO KWA VIONGOZI KUZINGATIA MISINGI YA UTAWALA BORA WAKATI WA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
Afisa Mwandamizi kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bi. Jovina Muchunguzi amebainisha changamoto mbalimbali zinazowasilishwa mara kwa mara na wananchi katika ofisi za Tume, akijibu swali lililoulizwa na mwendesha mjadala kutoka HakiRasilimali kuhusu changamoto zinazohusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Swali ambalo limeulizwa wakati wa mjadala katika Jukwaa la Uziduaji 2026 ulifanyika Leo Novemba 13, 2026.
Akibainisha changamoto hizo, Bi. Mchunguzi amesisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya utawala bora ambayo ni pamoja na uwazi, ushirikishwaji wa wananchi, uwajibikaji na utekelezaji wa shughuli kwa wakati, akieleza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika masuala yanayohusu maendeleo yao.
Miongoni mwa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara ni kukosekana kwa ushirikishwaji wa wananchi, mifumo ya kiutendaji kutokuwiana. pamoja na wahusika wa miradi kutotenga muda wa kutosha kutoa elimu na kueleza manufaa ya miradi kwa jamii husika. Hali hiyo husababisha wananchi kukosa uelewa wa kutosha na wakati mwingine kupoteza imani na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Aidha, ameeleza kuwa changamoto nyingine ni utekelezaji usioridhisha wa sheria na mifumo iliyowekwa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mikutano ya mara kwa mara kati ya watekelezaji wa miradi na wananchi ili kutoa taarifa, kujibu hoja na kufafanua masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa miradi hiyo.
Bi. Jovina amesema uwajibikaji, uwazi, ushirikishwaji na kuzingatia muda ni miongoni mwa misingi muhimu ya utawala bora ambayo inapotekelezwa kwa uaminifu husaidia kulinda haki za wananchi, kujenga imani kati ya jamii na watekelezaji wa miradi na kuhakikisha shughuli za maendeleo zinafanyika kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
Jukwaa la 11 la Uziduaji 2026 limefanyika kwa siku mbili, Novemba 12 na 13, 2026 katika Ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma, likiwa limeandaliwa chini ya HakiRasilimali kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali.

