THBUB NA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA ZANZIBAR ZAAHIDI KUDUMISHA USHIRIKIANO
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Wakili Dunford George Mpelumbe amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora (SMZ), Mhe. Haroun Ali Suleiman ofisini kwake eneo la Mazizini, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi Novemba 16, 2026. Katika ziara hiyo Mhe. Wakili Mpelumbe ameambatana na Makamu Mwenyekiti, Mhe. Omar Ali Omar Bhai na Naibu Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Bw. Juma Karibona.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mpelumbe amesisitiza kuwa THBUB ipo tayari kufanya kazi na kuendeleza ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Tume na Wizara hiyo.
Mhe. Wakili Mpelumbe ameeleza kuwa Tume imejipanga kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa weledi, ikiwemo kutoa elimu kwa umma na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa haki na bila upendeleo.
Kwa upande wake, Mhe. Haroun Ali Suleiman amewapongeza Mhe. Wakili Mpelumbe na Mhe. Omar Ali Omar kwa kuaminiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza chombo hicho muhimu cha kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.
Aidha, Mhe. Suleiman amewahakikishia viongozi hao kuwa Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa THBUB ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi visiwani Zanzibar.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara zinazofanywa na uongozi mpya wa THBUB, Mwenyekiti na Makamu wake kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau mbalimbali wa Serikali kwa lengo la kujitambulisha mara baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni.

