THBUB NA MAHAKAMA KUU ZANZIBAR KUIMARISHA USHIRIKIANO
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na Mahakama katika kulinda haki za binadamu na kusimamia misingi ya utawala wa sheria.
Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Wakili Dunford George Mpelumbe ameyasema hayo Novemba 18, 2026 alipomtembelea Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla katika ofisi za Mahakama Kuu, Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi visiwani humo.
Akieleza kuhusu ushirikiano huo, Mhe. Wakili Mpelumbe amesema Tume inatambua mchango wa Mahakama katika kusimamia utawala wa sheria na itaendelea kushirikiana nayo, hususan katika kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na kushughulikia malalamiko ya wananchi.
Kwa upande wake, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amepongeza uongozi mpya wa THBUB kwa kuteuliwa na kueleza kuwa Mahakama Kuu ya Zanzibar ipo tayari kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, bila upendeleo na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Viongozi hao wamejadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa kikazi baina ya taasisi hizo, kwa lengo la kulinda haki za binadamu na kuboresha mifumo ya utoaji haki ili iwe jumuishi na yenye ufanisi.
Mwenyekiti wa THBUB ameambatana na Makamu Mwenyekiti, Mhe. Omar Ali Omar Bhai, pamoja na Naibu Katibu Mtendaji, Bw. Juma Msafiri Karibona. Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za uongozi mpya kujitambulisha kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na taasisi za sheria visiwani humo, kufuatia kuteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

