THBUB, DIHR KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA ULINZI WA HAKI ZA BINADAMU
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Wakili Dunford George Mpelumbe amesema ushirikiano kati ya Tume hiyo na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark (DIHR) umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha juhudi za kukuza na kulinda haki za binadamu nchini, hususan katika masuala ya biashara na haki za binadamu pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari.
Mhe. Wakili Mpelumbe ameyasema hayo alipokutana na ujumbe wa DIHR uliojumuisha Bi. Katrina V. Palad, Mshirika wa Biashara na Mdhibiti wa Miradi pamoja na Bw. Bernard Ochieng, Mshauri wa Haki za Binadamu, Biashara na Teknolojia katika Ofisi za tawi za tume hiyo zilizopo Jijini Dar es Salaam Novemba 17, 2026.
Amesema ushirikiano huo ulioanza mwaka 2017 umewezesha Tume kutekeleza afua mbalimbali, zikiwemo kufanya Tathmini ya Hali ya Biashara na Haki za Binadamu nchini, kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu, kujenga uwezo wa watumishi na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji pamoja na upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki zinazohusiana na shughuli za biashara.
“Tunathamini sana ushirikiano wa muda mrefu na wa kimkakati kati ya taasisi zetu mbili, ambao umechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza na kulinda haki za binadamu nchini ,” amesema Mhe. Wakiki Mpelumbe.
Aidha, Mhe. Wakili Mpelumbe ameswma kuwa katika eneo la usimamizi wa rasilimali za bahari, Tume imefanya uchambuzi kuhusu haki za wavuvi wadogo na upatikanaji wao wa rasilimali za baharini kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu. Juhudi hizo zimechangia kuongeza uelewa wa jamii za pwani kuhusu haki zao, ushiriki katika maamuzi na mifumo ya kuwasilisha malalamiko na kupata suluhu.
Kwa upande wake, Bw. Bernard Ochieng amempongeza Mwenyekiti wa THBUB pamoja na Makamu Mwenyekiti kwa uteuzi walioupata, akiwatakia mafanikio katika majukumu yao. Pia, ameishukuru Tume kwa ushirikiano mzuri uliowezesha DIHR kutekeleza shughuli zake kwa mafanikio, huku akiahidi kuendeleza ushirikiano huo wenye tija.
Akizungumzia hatua zinazopaswa kupewa kipaumbele katika ulinzi wa haki za binadamu Mhe. Mpelumbe amesisitiza umuhimu wa kuharakisha kupitishwa na kuanza kutekelezwa kwa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki za Binadamu, kuimarisha mifumo ya kushughulikia malalamiko na kuhakikisha masuala ya haki za binadamu na mazingira yanazingatiwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Amesema Tume itaendelea kusimamia na kuimarisha misingi ya ulinzi wa haki za binadamu, uwajibikaji, upatikanaji wa haki na utawala jumuishi, ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanaenda sambamba na kuheshimu utu na haki za kila mwananchi

