HAKI ZA WATOTO WANAOLELEWA VITUONI KULINDWA.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa wito kwa vituo vinavyolea watoto wanaoishi katika mazingira magumu kuhakikisha haki za watoto zinalindwa kwa ufasaha.
Hayo yameelezwa wakati THBUB ilipotembelea Kituo cha Kulea Watoto cha Safina Street Network, Jijini Dodoma, kwa lengo la kufanya tathmini ya uzingatiwaji wa haki za watoto katika vituo vya malezi.
Akiongea katika kituo hicho Afisa wa THBUB, Bi. Florence Chaki amesema watoto wanaolelewa katika vituo wanapaswa kupata na kufurahia haki zao za msingi kama ilivyo kwa watoto wengine. “Watoto waliopo katika vituo vya kulea wanapaswa kutambuliwa na kulindwa kwa kupewa haki zao za msingi, ikiwemo haki ya kupata elimu, afya, malezi na ulinzi dhidi ya aina zote za ukatili,” amesema Bi. Chaki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Bw. Adam Wilson, amesema watoto wanaolelewa katika kituo hicho wanapata huduma muhimu ikiwemo elimu, chakula, malazi na fursa za kushiriki katika michezo. “Tunajitahidi sana kuhakikisha hawa watoto wanaishi kama watoto wengine waliopo katika familia zao,” amesema Bw. Wilson.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bi. Beatrice Lyimo, amesema kwa sasa wanatoa huduma kwa pamoja kwa kushirikiana na maafisa ustawi wa jamii kutoka Jeshi la Polisi, hospitali pamoja na vituo vya kulea watoto, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika kuwahudumia na kuwalinda watoto.
Amesema ushirikiano huo unasaidia kuhakikisha watoto wanaopitia mazingira magumu wanapata huduma zinazohitajika kwa wakati, huku hatua stahiki zikichukuliwa pale ambapo haki zao zinakiukwa.
Kituo cha Safina Street Network kinawahudumia watoto kutoka katika makundi mbalimbali, wakiwemo watoto waliotelekezwa, waliofanyiwa ukatili pamoja na watoto wa mitaani, kwa lengo la kuwapatia mazingira salama ya malezi na kuwawezesha kupata huduma muhimu kwa ajili ya ustawi wao.

