MAKAMU MWENYEKITI ATOA WITO KWA WANANCHI KUENDELEA KUWA NA IMANI NA THBUB
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewahakikishia Watanzania kuwa imejipanga kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku ikiwataka wananchi kuimarisha imani kwa Tume hiyo kwa kuwasilisha changamoto na malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili yaweze kushughulikiwa.
Wito huo umetolewa Novemba 9, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Mhe. Omar Ali Bhai, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Dunford George Mpelumbe na watumishi wa Tume Tawi la Dar es Salaam, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya THBUB Tawi la Dar es Salaam.
Akizungumzia mwelekeo wa THBUB katika kutekeleza majukumu yake, Mhe. Bhai amesema Tume imejipanga kutekeleza kwa vitendo maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kuwaapisha viongozi wa Tume hiyo, hususan agizo la kutosubiri malalamiko ya wananchi pekee, bali kuchukua hatua za kutambua na kushughulikia changamoto zinazohusu haki za binadamu na utawala bora kwa wakati.
“Kama mlivyosikia katika uapisho wetu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupatia maagizo muhimu, ikiwemo kutosubiri malalamiko ya wananchi. Sisi kama Tume tumejipanga kwa dhati na tutahakikisha tunafikia malengo ya Tume,” amesema Bhai.
Bw. Bhai amesema THBUB imejipanga kutumia njia mbalimbali kuwafikia wananchi na kupokea changamoto zao, ikiwemo mifumo ya kidijitali inayowawezesha kuwasilisha malalamiko bila kulazimika kufika moja kwa moja katika ofisi za Tume. Aidha, amebainisha kuwa mashauri yanayowasilishwa hupokelewa na kufanyiwa kazi kwa kuzingatia taratibu na mamlaka ya Tume.
Amesisitiza kuwa THBUB ni chombo cha wananchi, hivyo wanapaswa kuwa huru kuifikia na kuwasilisha changamoto zinazowakabili, zikiwemo zinazohusu ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, akiwahakikishia kuwa Tume itaendelea kutekeleza wajibu wake katika kushughulikia masuala hayo.
“Niwaomba wananchi wawe. na imani na Tume. Tutaendelea kushirikiana na wananchi wote. Vilevile, naomba vyombo vya habari, kama wadau wetu, viendelee kutoa taarifa mbalimbali na kushirikiana nasi katika kufanikisha malengo ya Tume,” ameeleza Bhai.
Ameongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuifikia jamii, kuelimisha umma na kuibua masuala yanayohusu haki za binadamu na utawala bora. Hivyo, amevitaka kuendelea kutumia nafasi hiyo kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia wananchi kufahamu haki zao, wajibu wao na namna ya kuifikia Tume wanapokabiliwa na changamoto.
Wito wa THBUB kwa wananchi kuendelea kuiamini Tume unaakisi dhamira ya kuimarisha uhusiano wake na jamii na kuhakikisha kuwa masuala ya haki za binadamu na utawala bora yanapewa kipaumbele. Tume inaendelea kuhimiza wananchi kutumia fursa zilizopo kuwasilisha changamoto zao ili ziweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria na mamlaka iliyopewa

