THBUB YAIMARISHA USHIRIKIANO PEMBA
Viongozi wakuu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Wakili Danford George Mpelumbe, akiambatana na Makamu Mwenyekiti, Mhe. Omar Ali Omar, wamefanya ziara ya kikazi kisiwani Pemba kwa lengo la kuitambulisha Tume na kuimarisha ushirikiano na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ngazi za Mkoa na Wilaya.
Katika ziara hiyo, viongozi hao wamekutana na Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Mhe. Zuhura Mgeni, na kumweleza majukumu ya Tume kwa mujibu wa Katiba, huku wakijadili namna ya kushirikiana katika kukuza, kulinda na kutetea haki za binadamu pamoja na misingi ya utawala bora.
Aidha, ujumbe huo umekutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Pemba, Bw. Amour Hamad, na kujadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tume na Ofisi ya Mkoa ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Tume na kuongeza ufanisi wa huduma zinazowafikia wananchi katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora.
Vilevile, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wametembelea ofisi za THBUB Tawi la Pemba zilizopo Kichungwani, Wilaya ya Chake Chake, na kufanya kikao kazi na watumishi wa tawi hilo kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza na watumishi hao, Mhe. Wakili Mpelumbe amesisitiza umuhimu wa kuwafikia wananchi katika maeneo yao ili kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, badala ya kusubiri wananchi wafike ofisini kutafuta huduma.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti ameunga mkono wito huo, akieleza umuhimu wa watumishi kuwa karibu na wananchi ili kurahisisha upokeaji na uchunguzi wa malalamiko pamoja na kubaini viashiria vya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa wakati.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Tume za kuimarisha ushirikiano na viongozi wa Serikali pamoja na kusogeza elimu na huduma za haki za binadamu na utawala bora karibu zaidi na wananchi.

