MPELUMBE ATETA NA LUGANGIRA KUHUSU UKATILI ARUMERU.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Wakili Dunford George Mpelumbe ameahidi kuimarisha ushirikiano na uongozi wa Wilaya ya Arumeru katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za binadamu .
Ahadi hiyo ameitoa Novemba 26, 2016, alipokutana na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Lugangira katika ofisi za wilaya hiyo zilizopo eneo USA river Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.
Katika kikao hicho, Mhe. Lugangira ameeleza kuwa ushirikiano wa wilaya hiyo na THBUB katika kukabiliana na matukio ya ukatili ni hatua muhimu kwa sababu Wilaya ya Arumeru ni miongoni mwa wilaya zenye idadi kubwa ya matukio ya ukatili , hali inayohitaji jitihada za pamoja kukabiliana nayo.
Aidha, Mhe. Wakili Mpelumbe amesisitza kuwa tume itatekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kutosubiri wananchi kuwasilisha malalamiko, bali kuwafuata walipo ili kubaini na kushughulikia changamoto zao.
“Hatutasubiri tu wananchi walete malalamiko ndipo tuchukue hatua, bali Tume imejipanga kuwafuata wananchi katika maeneo yao ili kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusu haki za binadamu,” amesema Mhe. Wakili Mpelumbe.
Kwa upande wake, Mhe. Lugangira amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na Tume katika kutoa elimu kwa jamii na kukabiliana na vitendo vya ukatili. “Tunahitaji nguvu ya pamoja katika kutoa elimu ya haki za binadamu, kwani bado kuna mila na desturi zinazochangia ukandamizaji wa haki za baadhi ya makundi katika jamii,” amesema Lugangira.
Katika hatua nyingine, Mhe. Wakili Mpelumbe amesema kuwa Tume ina mpango wa kufungua ofisi jijini Arusha ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika kulinda na kutetea haki za binadamu.

