THBUB YAHIMIZA KUVUNJA UKIMYA DHIDI YA UKATILI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Tawi la Mwanza, imetoa wito kwa wananchi kuvunja ukimya na kuripoti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Wito huo umetolewa kupitia kipindi cha Tuongee Asubuhi kilichorushwa na Star TV, Novemba 25, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake.
Katika kipindi hicho, THBUB imewakilishwa na Afisa Uchunguzi Mkuu, Bw. Chrisantus Ndibaiukao, na Afisa Sheria, Bi. Naomi Tesha, waliozungumzia haki za binadamu, ukatili wa kijinsia, wajibu wa jamii katika kuzuia vitendo hivyo na nafasi ya Tume katika kupokea na kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Akizungumza katika kipindi hicho, Bi. Tesha amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuficha au kuvumilia vitendo vya ukatili, bali wanapaswa kuviripoti na kuhakikisha waathirika wanapata msaada na haki stahiki.
“Ukatili dhidi ya wanawake na watoto haupaswi kufichwa wala kuvumiliwa. Kila mmoja ana wajibu wa kuvunja ukimya, kuripoti vitendo vya ukatili na kuhakikisha waathirika wanapata msaada na haki stahiki,” amesema.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Tuungane Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana: Hakikisha Haki Inatendeka, Linda Waathirika na Komesha Kutoadhibiwa kwa Watekelezaji wa Ukatili.”
Ushiriki huo ni sehemu ya juhudi za THBUB za kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu haki za binadamu na kuhamasisha jamii kushiriki katika kuzuia na kupinga vitendo vya ukatili.

