SKAUT DODOMA WAPATIWA ELIMU YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA.
Wanachama wa Skauti Dodoma wamepatiwa elimu ya haki za binadamu na utawala bora walipotembelea banda la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni Jijini Dodoma.
Wanachama hao walipatiwa elimu kuhusu haki mbalimbali zikiwemo haki ya kuishi, usawa mbele ya sheria, elimu, afya, kumiliki mali, uhuru wa kutoa maoni na elimu kuhusu misingi ya utawala bora.
Akitaja baadhi ya misingi ya utawala bora, Kaimu Mkurugenzi sehemu ya Utafiti na Nyaraka THBUB, Bw. Paul Sulle alisema misingi hiyo imewekwa ili kuhakikisha jamii inaishi katika amani na haki.
"Uwazi , ushirikishwaji, usawa mbele ya sheria na uwajibikaji ni miongoni mwa nguzo muhimu za misingi ya utawala bora" amesema Bw. Sulle.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama hao Godfrey Elia ameishauri THBUB kuwa na mkakati wa kutoa elimu kwa wanachama wa Skauti nchi nzima ili kuwaongezea uelewa zaidi wa masuala ya haki za binadamu na utawala bora.

