TAHILISO UDOM WAAHIDI KUWA MABALOZI WA HAKI ZA BINADAMU BAADA YA KUPATIWA ELIMU NA THBUB.
Uongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa elimu ya Juu (Vyuo vya kati na Vyuo Vikuu) Tanzania (TAHILISO) kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), leo umetembelea Ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) zilizopo katika Jengo la PSSSF, Mtaa wa Makole jijini Dodoma, kwa lengo la kujifunza kuhusu majukumu, mamlaka na shughuli zinazotekelezwa na THBUB katika kulinda, kuhifadhi na kutetea haki za binadamu pamoja na kuhimiza misingi ya utawala bora nchini.
Viongozi hao wamepokelewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma, Mawasiliano, Tafiti na Nyaraka wa THBUB, Bw. Paul Sulle, ambaye amewaeleza dhamira ya THBUB ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za elimu ya juu kupitia programu mbalimbali za utoaji elimu, ikiwemo kuanzisha vilabu vya haki za binadamu na utawala bora, mashindano ya ubunifu na midahalo katika vyuo mbalimbali kwa kushirikiana na TAHILISO.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Kamishna wa Uongozi wa TAHILISO, Bi. Upendo Jonathan, amesema elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu majukumu ya THBUB na umuhimu wa taasisi hiyo katika kulinda haki za binadamu na UTAWALA bora nchini. Ameahidi kuwa TAHILISO itaendelea kushirikiana na THBUB katika kutoa elimu kwa wanafunzi na jamii, huku wanafunzi wa sheria wakitimiza wajibu wao wa kuwa mabalozi wa haki za binadamu na utawala bora.
Kwa upande wake, Afisa Mchunguzi kutoka Idara ya Elimu kwa Umma, Mawasiliano, Tafiti na Nyaraka wa THBUB, Bw. David Piniel, amewaeleza vuongozi hao kuwa THBUB ni taasisi huru ya kikatiba na kisheria iliyoanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 129(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kupewa mamlaka ya kutekeleza majukumu yake kupitia Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sura ya 391.
Bw. David amefafanua kuwa THBUB ina jukumu la kulinda, kukuza na kutetea haki za binadamu, kuhimiza misingi ya utawala bora, kupokea na kuchunguza malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, kufanya uchunguzi, kutoa mapendekezo kwa mamlaka husika pamoja na kuendesha programu za elimu kwa umma.
Aidha, amewahimiza vuongozi hao kupeleka ujumbe kwa wanafunzi kutumia taaluma yao kuelimisha jamii, kuhamasisha matumizi ya njia halali za kutafuta haki na kushiriki katika kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria na misingi ya utawala bora.
Ziara hiyo inaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya THBUB na taasisi za elimu ya juu katika kukuza elimu ya haki za binadamu na utawala bora. Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu HAKI na wajibu wao katika kulinda na kutetea haki za binadamu na kuwa sehemu ya kujenga jamii yenye haki, usawa na uwajibikaji.

