THBUB YAENDELEA KUTOA ELIMU KWA JAMII KUHUSU ULINZI WA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na kuheshimu haki za binadamu kupitia vyombo vya habari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao.
Akizungumza leo Julai 16, 2026 kupitia kipindi cha Mwanga wa Asubuhi kinachorushwa na Radio Missionaries FM Dodoma, Afisa Uchunguzi Mkuu Msaidizi wa THBUB, Bw. Halfan Botea , amesema kuwa haki za binadamu ni haki za msingi zinazostahili kuheshimiwa na kulindwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Bw. Botea amefafanua kuwa haki ya kuishi ni miongoni mwa haki zinazokiukwa mara kwa mara, hivyo ametoa wito kwa wananchi kuheshimu sheria na kuepuka vitendo vinavyohatarisha maisha ya wengine.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanawake na watoto wanapata ulinzi wa kisheria dhidi ya ukatili, unyanyasaji na ubaguzi.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu kupitia utekelezaji wa Katiba, sheria, sera na taasisi zinazosimamia haki na utoaji wa haki.
" jitihada hizo zinahitaji kuungwa mkono na wananchi kwa kuheshimu sheria pamoja na kushirikiana na mamlaka husika katika kuzuia na kuripoti vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu"amesema Bw.Botea
Aidha, Bw.Botea ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika pindi haki zao zinapokiukwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
THBUB imeendelea kutumia njia mbalimbali ya mawasiliano kutoa elimu kwa umma ili kujenga jamii inayotambua haki zake, kutekeleza wajibu wake na kuimarisha utawala bora nchini.

