THBUB YASISITIZA UTOAJI WA HAKI BILA UBAGUZI.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesisitiza kuwa kila mwananchi anayefika mbele ya Tume hiyo anapokelewa na kuhudumiwa kwa usawa, heshima na bila ubaguzi, kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora.
Kauli hiyo imetolewa Julai 11, 2026 na Afisa Uchunguzi Mkuu wa THBUB, Bi. Neema Kafanabo alipokuwa akipokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi waliotembelea banda la THBUB kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SabaSaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Bi. Kafanabo amesema THBUB imejipanga kuhakikisha kila mwananchi, bila kujali jinsia, umri, hali ya kiuchumi, ulemavu, dini au asili yake, anapata fursa sawa ya kusikilizwa na kushughulikiwa lalamiko lake lililofikishwa katika ofisi zote za taasisi hiyo.
"Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ipo kwa ajili ya wananchi wote. Kila anayefika kwetu anasikilizwa kwa heshima, anapewa huduma kwa usawa na malalamiko yake yanapokelewa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria bila upendeleo," amesema Bi. Kafanabo.
Bi. Kafanabo ametoa wito kwa wananchi wengine wenye malalamiko yanayohusu uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora wasisite kuyawasilisha THBUB, kwani taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa mujibu wa sheria.
Naye Bw. Rashid Khatibu aliyefikisha lalamiko lake mbele ya Tume, ameeleza kufurahishwa na kupongeza kwa namna alivyopokelewa, kusikilizwa na lalamiko lake kuanza kushughulikiwa kwa haraka. Amesema amejionea kuwa Tume inatekeleza kwa vitendo wajibu wake wa kusimamia haki za binadamu na kuimarisha misingi ya utawala bora.
"Nilifika nikiwa na hofu kama nitasikilizwa, lakini nimepokelewa kwa heshima na suala langu limeanza kufanyiwa kazi mara moja. Nimeona kwa macho yangu kuwa Tume inawahudumia wananchi wote kwa usawa na haisiti kusimamia haki bila kujali taasisi au mamlaka inayohusika. Hii ndiyo tafsiri halisi ya utawala bora," amesema Bw. Rashid.
Aidha, THBUB imeendelea kutumia Maonesho ya SabaSaba kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu, wajibu wa wananchi, ushauri wa kisheria na kupokea malalamiko, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha huduma zinawafikia Watanzania wote kwa usawa, uwazi na haki.

