THBUB NA JESHI LA POLISI WAKUTANA KUJADILI KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO YA THBUB.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Jeshi la Polisi wamejadili namna Jeshi hilo lilivyotekeleza mapendekezo yaliyowasilishwa katika Jeshi hilo yaliyotokana na Chunguzi zilizofanywa na THBUB. Majadiliano hayo yamejiri katika kikao kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jijini Dodoma Juni 18, 2026.
Akifungua kikao hicho, Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB ambaye pia ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Bi. Suzan P. Ndeona, amesema kuwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi ni nguzo muhimu ya kuibua matukio ya uvunjifu wa amani, kuibua matukio ya kiuhalifu sambamba na kuwasaidia wananchi katika kuwapatia elimu kuhusu haki na wajibu wao.
“ushirikiano huo utasaidia kuimarisha imani ya jamii kwa vyombo vya dola” amesema Bi. Ndeona.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Peter Lusesa amekiri kupokea malamiko ya uwepo kwa baadhi ya vitendo vinavyolichafua jeshi hilo ikiwemo matumizi ya nguvu dhidi ya raia, vitendo vya ukatili na malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu. Amesema hali hiyo imechangia baadhi ya wananchi kupoteza imani kwa jeshi hilo.
Akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii, ACP Lusesa amesema Polisi ni watu na watu ni polisi hivyo ushirikiano na jamii ni jambo la msingi.
Pia amesisitiza kuwa usalama wa nchi unategemea ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya usalama.
Kikao hicho pia kimejadili changamoto za rushwa, unyanyasaji wa wananchi, pamoja na maelewano hafifu kati ya wananchi na Polisi wa Uhifadhi.
Aidha, washiriki wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwajibikaji na kuheshimu haki za binadamu katika utoaji wa huduma za kipolisi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Taasisi za Haki Jinai kutokaTHBUB, Bw. Constantine Mugusu, ameliomba Jeshi la Polisi kuongeza matumizi ya kamera za ulinzi barabarani na kuongeza vituo vya Polisi ili kuboresha huduma na kupunguza msongamano wa watuhumiwa katika vituo vilivyopo.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa pande zote mbili kukubaliana kuimarisha ushirikiano, uwajibikaji na kuendeleza misingi ya haki za binadamu na utawala bora nchini.

