ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI KWA MANUFAA YA WANANCHI

18 Jun, 2026
WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI KWA MANUFAA YA WANANCHI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb) amewataka watumishi wa umma nchini kuimarisha utendaji kazi ili kuongeza tija katika kufikia malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi.

Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma kuanzia Juni 16 hadi 23, 2026.

Amesema maadhimisho hayo yanalenga kuongeza uelewa kuhusu huduma zinazotolewa katika utumishi wa umma, kuhimiza matumizi ya mifumo ya utoaji huduma, kutoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi na watumishi, pamoja na kupata mrejesho kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma.

Mhe. Kikwete amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa watumishi wa umma kutafakari utekelezaji wa majukumu yao, kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya za utoaji huduma na kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza katika utendaji kazi, hatua ambazo huchangia kuleta mageuzi na kuimarisha huduma kwa wananchi.

Aidha, amesema maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, akieleza kuwa kaulimbiu hiyo inapaswa kuwa chachu ya kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma kwa manufaa ya wananchi.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utumishi wa umma kupitia maeneo muhimu ya mabadiliko ya fikra, ushirikishwaji wa wananchi, uongozi na uwajibikaji, usimamizi wa rasilimali watu pamoja na mageuzi ya huduma za kidijitali ili kukidhi mahitaji ya wananchi kwa ufanisi zaidi.

Pia ametoa wito kwa watumishi wa umma kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji, uadilifu na uzalendo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi, amesema Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yalianzishwa mwaka 2021 kwa lengo la kutambua mchango wa watumishi wa umma katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Maadhimisho hayo yanaendelea kutoa jukwaa muhimu la kuimarisha uwajibikaji, kuboresha utoaji wa huduma na kujenga utumishi wa umma unaozingatia mahitaji ya wananchi, sambamba na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.

slot gacor