THBUB: WALIMU WALEZI MSIFUMBIE MACHO UKATILI DHIDI YA WATOTO
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka walimu walezi wa Klabu za Haki za Binadamu kuwa mstari wa mbele katika kutambua, kuzuia na kuripoti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, ndani na nje ya mazingira ya shule.
Wito huo umetolewa na Bi. Shoma Philip, Afisa Mfawidhi wa THBUB, Tawi la Dar es Salaam, wakati akifungua mafunzo elekezi kwa walimu walezi wa klabu hizo kutoka Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkuranga, Oktoba 15, 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bi. Shoma amesema watoto wengi wanaishi katika mazingira hatarishi na wakati mwingine watu wanaowazunguka, wakiwemo majirani, huhusika na vitendo vya ukatili dhidi yao. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa walimu na jamii kuwa makini katika kuwalinda watoto na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.
“Kama walimu walezi tuna jukumu la kuhakikisha macho yetu wote tunayaelekeza kwa watoto. Watoto wengi wanaishi katika mazingira hatarishi ambapo majirani zetu ndio wanaowatendea vitendo vya kikatili,” amesema.
Ameongeza kuwa uelewa wa haki za binadamu utawawezesha walimu walezi kutambua viashiria vya ukiukwaji wa haki za watoto, kuwapa elimu kuhusu haki na wajibu wao na kuripoti matukio ya ukatili kwa mamlaka husika. Amesisitiza, “Walimu walezi, mkizifahamu haki za binadamu vizuri, mtakuwa msaada mkubwa kwetu na kwa watoto mashuleni na hata kwenye jamii zetu.”
Kwa upande wake, Mwalimu Mark M. Tesha kutoka Shule ya Sekondari Mwarusembe ameishukuru THBUB kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yatasaidia kuongeza uelewa wa walimu kuhusu haki za binadamu na kuimarisha utekelezaji wa majukumu yao katika Klabu za Haki za Binadamu. Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza elimu itakayowawezesha wanafunzi kutambua haki zao na kuripoti vitendo vya ukatili.
Mafunzo hayo yenye lengo la kuimarisha uwezo wa walimu walezi katika kuendesha klabu hizo na kujenga mazingira salama yanayoheshimu haki, utu na ustawi wa watoto, yalihitimishwa kwa kaulimbiu isemayo “Ona, Hisi, Chukua Hatua,” inayohamasisha jamii kutambua viashiria vya ukiukwaji wa haki za binadamu, kujali waathirika na kuchukua hatua stahiki kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

