THBUB YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA KIKE KWA KUWAJENGEA UWEZO WANAFUNZI WA BUTIMBA A NA B
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Tawi la Mwanza, imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike kwa kutoa elimu kwa wanafunzi wa kike wa Shule za Msingi Butimba A na Butimba B jijini Mwanza, kuhusu haki zao, wajibu wao, ulinzi dhidi ya ukatili na umuhimu wa kujiamini katika kufikia ndoto zao.
Maadhimisho hayo yamewashirikisha wanafunzi hususani wa kike pamoja na walimu walezi wa klabu za Haki za binadamu.
Lengo kuu la maadhimisho ni kuwajengea uelewa wadau hao kuhusu haki za msingi za mtoto.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Maafisa kutoka THBUB walisisitiza kuhusu umuhimu wa kujithamini, kuheshimu wengine na kutambua mahali pa kupata msaada wanapokabiliwa na vitendo vinavyokiuka haki zao.
Mada zilizowasilishwa zilijumuisha haki za mtoto wa kike, usawa wa kijinsia, ulinzi dhidi ya ukatili, kujiamini, wajibu wa mtoto na nafasi ya klabu za haki za binadamu katika kujenga mazingira salama shuleni.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Bi. Naomi Tesha, Afisa Sheria wa Tume, alisisitiza umuhimu wa mtoto wa kike kufahamu haki zake “Mtoto wa kike anapaswa kufahamu kuwa ana haki, ana thamani na ana uwezo wa kufikia ndoto zake. Ni wajibu wa wazazi, walimu na jamii kuhakikisha anakuwa katika mazingira salama yanayomwezesha kujifunza, kujiamini na kushiriki kikamilifu katika maendeleo yake.” Alisema Bi. Naomi Tesha
Kwa upande wake, Mwl. Violeth Shio, mwalimu mlezi wa klabu, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya haki za binadamu shuleni ili kuwasaidia wanafunzi kutambua haki na wajibu wao. Alieleza kuwa ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wadau kama THBUB ni muhimu katika kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa na wanapata fursa ya kuendeleza uwezo wao. “Elimu hii ni muhimu kwa wanafunzi wetu kwa sababu inawasaidia kutambua haki zao, kujua wajibu wao na kuelewa namna ya kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili. Tuna wajibu wa kuendelea kuwaongoza na kuhakikisha shule inakuwa sehemu salama kwa kila mtoto.”
Naye mmoja wa wanafunzi walioshiriki katika shughuli hiyo aliishukuru Tume kwa kutembelea shule zao na kuwapatia elimu kuhusu haki za mtoto wa kike. Alisema wamejifunza mambo mengi yatakayowasaidia katika maisha yao ya kila siku. “Tunashukuru sana THBUB kwa kuja shuleni kwetu na kutufundisha mambo mengi kuhusu haki na wajibu wetu. Tumejifunza jinsi ya kujithamini, kujilinda na kuheshimu wengine. Tutaendelea kuyazingatia na kuyaishi yale tuliyojifunza katika mazingira yetu ya shule na nyumbani.”
Kupitia shughuli hiyo, THBUB imeendelea kuimarisha elimu ya haki za binadamu na utawala bora kwa watoto kupitia ushirikiano na shule pamoja na Haki Clubs. Tume inahimiza jamii kuendelea kumlinda mtoto wa kike, kuheshimu haki zake na kumpa fursa sawa za elimu na maendeleo ili aweze kukua katika mazingira salama na kutimiza ndoto zake.

