THBUB YASISITIZA ULINZI WA HAKI ZA BINADAMU KATIKA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA BAHARI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesisitiza umuhimu wa kulinda na kuzingatia haki za binadamu katika usimamizi na matumizi ya rasilimali za bahari ili kuhakikisha wananchi wanaozitegemea rasilimali hizo wanapata manufaa stahiki kwa maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla.
Msisitizo huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa THBUB, Bw. Patience Ntwina, wakati akifungua mafunzo kwa wanufaika wa mazao ya rasilimali za bahari pamoja na wasimamizi wa rasilimali hizo katika eneo la Msanga Mkuu, mkoani Mtwara.
Mafunzo hayo yanayoendelea kutolewa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Tanga yanalenga kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya bahari kuhusu usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, sambamba na kuhamasisha ushiriki wao katika kulinda haki za binadamu na mazingira. Washiriki pia wanapata fursa ya kujadili changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kiuchumi na kutafuta njia bora za kuzitatua kwa kuzingatia sheria na misingi ya haki za binadamu.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Bw. Ntwina amesema usimamizi bora wa rasilimali za bahari unapaswa kuzingatia haki na maslahi ya makundi yote yanayotegemea sekta hiyo, hususan wavuvi wadogo na jamii za maeneo ya pwani.
Amesema uchambuzi wa awali uliofanywa na THBUB unaonesha kuwa wavuvi wadogo wana mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha kaya, kutoa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo ya pwani. Aidha, sekta ya uvuvi inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhifadhi utamaduni na kuimarisha mshikamano wa kijamii kwa jamii zinazozunguka maeneo ya bahari.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fundikila Wazambi, amewataka wavuvi na wadau wengine wa rasilimali za bahari kutambua kuwa kulinda na kuheshimu haki za binadamu ni wajibu wa kila mwanajamii.
“Kila mvuvi anapaswa kutambua haki zake pamoja na mipaka ya haki hizo ili kuepuka kuingilia haki za watu wengine isipokuwa kwa mujibu wa sheria. Ni muhimu kuhakikisha shughuli zote za kiuchumi zinafanyika kwa kuzingatia sheria na kuheshimu haki za wengine,” amesema Fundikila.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru THBUB kwa kuwapatia elimu hiyo, wakieleza kuwa itawasaidia kutambua, kulinda na kutetea haki zao katika shughuli zao za kila siku, hususan katika sekta ya uvuvi.
Mafunzo hayo yanaakisi dhamira ya THBUB ya kuendeleza uelewa wa haki za binadamu katika usimamizi wa rasilimali za asili, kwa kuzingatia kuwa matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, ushiriki wa jamii na utawala unaozingatia haki ni nguzo muhimu katika kufikia maendeleo jumuishi na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu duniani.

