TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YASHIRIKI MAONESHO YA KILIMO NANE NANE KANDA YA MAGHARIBI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Kanda ya Magharibi inashiriki Maonesho ya Kilimo Nane Nane Kanda ya Magharibi yanayofanyika katika Viwanja vya Ipuli, mkoani Tabora, yenye kaulimbiu isemayo, "Tambua Soko, Zalisha kwa Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."
Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, Tume imeendelea kutoa elimu, ushauri na kufikisha huduma mbalimbali zinazohusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa wananchi wanaotembelea banda lake. Wananchi wengi wameonyesha kufurahishwa na ushiriki wa Tume, wakieleza kuwa elimu inayotolewa imewasaidia kuongeza uelewa kuhusu haki zao, wajibu wao pamoja na namna ya kupata huduma kutoka Tume.
Tume inaendelea kuhamasisha wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda lake ili kupata elimu, ushauri na ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu na utawala bora.
Maonesho ya Kilimo Nane Nane Kanda ya Magharibi yalizinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu, Balozi Simon Sirro, na yanatarajiwa kuendelea hadi Agosti 8, 2026, siku ambayo itakuwa kilele cha maonesho hayo.

