THBUB, WADAU WAJADILI HATUA ZA KUPUNGUZA VIFO NA MAGONJWA YANAYOWEZA KUZUILIKA KWA WAJAWAZITO
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imekutana na wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Afya, kujadili utekelezaji wa Azimio Na. 60/18 la Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia vifo na magonjwa ya akina mama yanayoweza kuzuilika, kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Utawala Bora wa THBUB, Bi. Suzan Ndeona, amesema kuwa lengo ni kupata taarifa, maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuzuia vifo na magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa wanawake wakati wa ujauzito na kujifungua, kwa kuzingatia haki za binadamu.
Bi. Ndeona ameeleza kuwa Azimio hilo, lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Oktoba 7, 2025, linasisitiza umuhimu wa kulinda haki za wanawake na kuhakikisha wanapata huduma bora za afya ya uzazi ili kupunguza vifo na magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Bi. Ndeona ameongeza kuwa taarifa na maoni yatakayokusanywa kupitia majadiliano hayo yatatumika kuandaa mpango wa THBUB utakaowasilishwa kwa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2027, kuhusu utekelezaji wa azimio hilo.
Aidha, katika kikao hicho, washiriki wameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuboresha huduma za afya ya uzazi, kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma bora, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini pamoja na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji katika utoaji wa huduma hizo.
Vilevile, washiriki wamebadilishana uzoefu kuhusu mafanikio yaliyopatikana, changamoto zinazoendelea kujitokeza na maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele zaidi katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Majadiliano hayo ni moja Ua hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau, kuhakikisha huduma za afya ya uzazi zinapatikana kwa usawa na ubora na kuweka mifumo madhubuti ya uwajibikaji ili kulinda haki ya kila mwanamke kupata huduma za afya zinazostahili. Hatua ambazo ni muhimu katika kuzuia vifo na magonjwa yanayoweza kuzuilika na kuhakikisha usalama na ustawi wa wanawake na watoto.

