THBUB YAIMARIISHA USHIRIKIANO NA OFISI YA MKOA WA MWANZA
Watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Tawi la Mwanza wamtembelea Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Fatuma Mganga kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo katika kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa THBUB ulipata fursa ya kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa taasisi hizio katika kushughulikia masuala yanayohusu haki za binadamu na utawala bora.
Aidha, THBUB ilitumia fursa hiyo kufuatilia utekelezaji wa malalamiko yaliyowasilishwa awali kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo . Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za THBUB katika kuhakikisha uhifadhi wa haki za binadamu.
Aidha, THBUB ilimkabidhi Dkt. Mganga vifaa vya uhamasishaji ikiwamo vipeperushi ya kuelimisha umma.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt Mganga alisema: “Ushirikiano baina ya taasisi za umma ni muhimu katika kuhakikisha masuala yanayowahusu wananchi yanashughulikiwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya haki na utawala bora.”
THBUB inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma na wadau wengine katika kutekeleza jukumu lake la kukuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu pamoja na kusimamia misingi ya utawala bora nchini.

